Ukiona nzi ameweza kutua katika jiko la mkaa, basi kwa urahisi
tu utajua kuwa hakuna moto juu ya jiko hilo. Vivyo hivyo kama ndani ya roho
yako hamna moto wa Roho Mtakatifu lazima mapepo watafanya makazi. Ili uweze
kupata moto wa Roho mtakatifu ndani yako ni lazima ujazwe Roho Mtakatifu na
upate muda wa kutosha wa kuomba kwa kunena kwa lugha.
Unapojazwa Roho Mtakatitifu, huwa haingii kwenye akili,
mawazo wala kwenye mwilini mwako bali huingia kwenye roho. Roho Mtakatifu
anapoingia ndani huwa anafanya mawasiliano na roho yako. Wakati roho ya
mwanadamu inapokuwa inafanya mawasiliano na roho mtakatifu hapo ndipo mtu huyo
anajikuta ananena kwa lugha; kwahiyo kunena kwa lugha ni udhirisho kuwa roho ya
mwanadamu ina fanya mawasiliano na Mungu. Na ndio maana moja ya udhihirisho
kuwa umeokolewa ni kunena kwa lugha (Marko 16:17), kwasababu ukiokoka Roho Mtakatifu
anaingia ndani yako.
Katika Biblia; kuna namna tatu ambazo watu walijazwa Roho
Mtakatifu; kama ifuatavyo:
i)
Kuomba mwenyewe:
Siku
ya pentekoste, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamekusanyika wakiwa wanaomba; (Matendo ya
Mitume 2:1-7), kumbe
namna ya kwanza ni kwa kuomba mwenyewe, yaani unakuwa unaomba alafu katikati ya
maombi Roho Mtakatifu anakuja ndani mwako na hapo unaanza kunena kwa lugha.
ii)
Kuwekewa mikono:
Namna
ya pili ya mtu kupokea Roho Mtakatifu kwenye Biblia ni kwa kuwekewa mikono,
tunaona katika (Matendo ya Mitume 19:6), Paulo aliwawekea mikono, na alipowawekea wote wakanena kwa lugha, kumbe
mtu anaweza kujazwa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu.
iii)
Kulisikia neno la Mungu linapohubiriwa:
Namna
nyingine ni kwa kusikiliza neno la BWANA; (Matendo ya Mitume 10:44), hapa tunaona Roho Mtakatifu
amewashukia watu wakati Petro alipokuwa akiongea, kumbe unaweza kupokea Roho
Mtakatifu kwa kusikiliza neno la Mungu, (Ezekieli 2:2); Mungu aliposema naye Roho
ikamwingia, ni kwa kusikiliza neno la Mungu.
Kuna vizuizi vinavyoweza kumzuia mtu asinene kwa lugha; Adui
wakuu watatu wanaomfanya mtu asinene kwa Lugha:
i)
Ujasiri:
Roho
mtakatifu ni Roho wa ujasiri, kwa hiyo unapoomba unatakiwa uombe kwa ujasiri. Unapokosa
ujasiri wakati kuomba, Roho mtakatifu hawezi kuingia (1Timotheo
1:7), Roho
mtakatifu si roho wa kusitasita wala woga bali ujasiri. Mtu aweza kushindwa
kunena kwa lugha kwasababu ya kukosa ujasiri.
ii)
Mapokeo:
Maarifa
uliyoyapokea zamani yanaweza kukuzuia kunena kwa lugha kwasababu inawezekana
kabla ya kuokoka mtu alikuwa ametokea katika dhehebu ambalo halineni kwa lugha,
nalo linaweza kuwa kikwazo, (Marko 7:8), maarifa ni jambo muhimu sana kwenye maendeleo ya mtu,
unapokosa maarifa sahihi ya neno la Mungu Roho Mtakatifu hawezi kuingia ndani
yako.
iii)
Hofu:
hofu
inaweza kukufanya ushindwe kupokea Roho Mtakatifu kwasababu ya kuogopa watu
watakuonaje, unawaza ukianza kuongea maneno yale watahisije, (Waebrania
10:38) hofu ni adui
mkubwa wa kunena kwa lugha kwasababu inakuzuia kujiachia mbele za Mungu.
Kunena kwa lugha ni njia mojawapo ya kufunguliwa kutoka
katika vifungo vya rohoni kwasababu unaponena kwa lugha, kimsingi; roho yako
inakuwa inawasiliana na Roho Mtakatifu. Na ndio maana nguvu za mtu za rohoni
zinategemeana sana na muda anaotumia kunena kwa lugha; kama ukinena kwa lugha
kwa saa moja basi utakuwa na upako wa saa moja. Nena kwa lugha muda wa kutosha.
Limetolewa kwenye moja ya masomo ya Mch. Josephat Gwajima:
No comments:
Post a Comment