GOD LOVES YOU/MUNGU ANAKUPENDA

Yohana 3:16 "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."

John 3:16 "For God so loved the world that he gave his one and only Son, that whoever believes in him shall not perish but have eternal life.

Sunday, August 26, 2012

UJUMBE : LAANA YA FAMILIA pt 2 26.8.2012

Na Mch. Kiongozi: JOSEPHAT GWAJIMA

Utangulizi:
Tuliangalia wiki iliyopita kuwa Baraka zaweza kurithishwa; Mithali 13:22 na kwa namna hiyo tukaona pia kuwa kama Baraka zaweza kurithishwa basi hata laana zaweza kurithishwa; Tukaona pia wazazi wazazi wanapotenda mema, wema huo huo hupita hadi kwa wana wa wanao 2Timotheo 1:3-5 kwa namna hii tukaona kuwa imani yaweza kupita kutoka kwa baba hadi kwa mototo:

Laana ni mashetani yaliyoagizwa kuja kwenye maisha, ukoo, familia n.k yaliyotumwa kuja kusimamia tatizo Fulani; laweza kuwa kutokuzaa, vifo vya mapema, magonjwa, umaskini na matatizo. Na kama vile Roho Mtakatifu husimamia neno litimie vivyo hivyo na mashetani yanasimamia ukae kwenye tatizo hilo ili laana iendelee kukaa. Kuna aina mbalimbali za laana.

FAMILIA YAWEZA KUWA CHINI YA LAANA:
Kila unalofanya leo zuri au baya lina athari kwako na kwa watoto wako pia; Na ndio maana wana wa Israeli kwa kulijua hili, baada ya pilato kunawa mikono kuwa hausiki kumsulibisha Yesu wao wakasema damu yake iwe juu yetu na watoto wetu; Mathayo 27:24-26 Wana wa Israeli walijua kuwa kama Yesu hana hatia basi lazima laana ipite kwenye maisha yao. 1 Petro1:18 Kimsingi imani yaweza kurithishwa, kutoka kwa mzazi hadi kwa watoto. Kama wazazi wakitenda uovu, ile laana yaweza kupita katika kizazi chake KUTOKA 34:5-8, Mungu anaweza kupitiliza laana katika ukoo kwasababu ya uovu.
Na ndio maana waweza kuwaona hata viongozi wa Tanzania; unakuta baba alikuwa kiongozi serikalini na mtoto wake pia uongozi unawafuata.

MATATIZO YANAYO FANANA:
Kumbukumbu 5:7-10; Laana yaweza kusababisha familia ikawa na matatizo yanayo fanana; na ndio maana waweza kukuta kwenye familia baba alikufa maskini na mtoto naye umaskini unamfuata; laana ya familia. Yeremia 32:17-18 “wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake;” Biblia iko wazi kuhusu swala hili, Mungu huwalipa wazazi uovu wao kupitia wana wao, na ndio maana mataifa mengi ya kiafrika ni maskini kwasababu mataifa yapo kwenye laana kwasababu ya aidha viongozi au historia ya huko nyuma.

Kipindi cha Yoshua alikuwepo mtu mmoja anaitwa Akani, aliyeliletea taifa zima la Israeli laana; kumbe taifa laweza kuingia kwenye laana kwasababu ya mtu mmoja Yoshua 7:24 “Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori. Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? Bwana atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.” Mtu mmoja aliingizia taifa zima laana, nchi yaweza pata laana kwasababu ya mtu mmoja.

MFANO WA NUHU NA WANAWE:
Nuhu baada ya kutoka kwenye safina akawa na watoto wake; baada ya kuishi kuna jambo likatokea la kushangaza ambalo kupitia hilo tutajifunza; Mwanzo 9:18 “Wana wa Nuhu waliotoka katika safina, ni Shemu, na Hamu, na Yafethi; na Hamu ndiye baba wa Kanaani.” Hapa tunaona kuwa Kanaani alikuwa mtoto wa Hamu; jambo la kushangaza ni kwamba Nuhu alilewa alafu akanywa kileo akalewa; akawa uchi alafu mwanaye ambaye ni Hamu akamwona akiwa uchi alafu akaenda kuwambia ndugu zake.

Lakini baada ya Nuhu kuelevuka kutoka katika ulevi, hakumlaani Hamu ambaye ndiye aliyeona lakini yeye akamlaani Kanaani, Mwanzo 9:25-26 “Akasema, Na alaaniwe Kanaani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe Bwana Mungu wa Shemu; Na Kanaani awe mtumwa wake.” Utajiuliza kwanini Mungu aruhusu kanani aliye mtoto wa Hamu kulaaniwa? Kimsingi; laana hupita katika watoto wa Hamu na ukoo wao lakini laana yao hii ilianzia kwa Hamu.

USHAHIDI WA LAANA YA KANAANI:
Kuthibitisha laana ya Kanaani tuangalie katika uzao wake; Mwanzo 10:15-20 “Kanaani akamzaa Sidoni, mwanawe wa kwanza, na Hethi, na Myebusi, na Mwamori, na Mgirgashi…,” Kumbe wana wa kanaani ndio hao. Na ili kuthibitisha hili emu atuangalie maandiko yafuatayo yanaonyesha

Kupata uthibitisho wa makabila ya watoto wa Kanaani katika kitabu Kutoka 3:8,17 23:23; 33:5; Hawa wote ndio wana wa Kanaani wayebushi n.k. kumbe mtu unaweza ukaamshangaa Mungu anawambia wana wa Israeli wawafukuze hawa kumbe ni kwasababu ya laana ya Hamu iliyokuwa tangu mwanzo hili jambo ni halisi kuwa laana hupita kwenye familia na biblia haibishanii hilo.

UOVU WA MTU WA LEO NI LAANA YA FAMILIA NA UKOO WAKE KESHO:
Mambo ya nyakati 4: 10 “Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.” Yabesi alijua kuwa jambo baya la leo laweza kumletea kilio kesho; na hivyo akaamua kumlingana BWANA akamwomba amuondolee laana. Uovu wa mtu ni laana yake kesho, na laana hii hupita hadi kwenye familia na ukoo wake.

Zakaria 5:1-4 “Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili. Nitaituma itokee, asema Bwana wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.” Laana yaweza kupaa kufuata familia, na ikiingia ina madhara makubwa. Jambo lolote walilotenda wazazi lina madhara kwa watoto;

MFANO WA MFALME SULEIMANI:

1Wafalme 11:1 “Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake...”

Ukiendelea kusoma hapo utaona Mfalme Suleimani alifikia kujenga madhabahu ya miungu mingine. Lakini jambo la kushangaza zaidi ni pale Mungu alipokuja kumpa hukumu akamwambia 1Wafalme 11:9-12 “Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana. Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.”

Ni jambo ambalo linaweza kuonekana ni la kawaida tu; lakini hili andiko la pili linatuonyesha kuwa wema aliotenda baba waweza kumwokoa mtoto; kwasababu ya mambo mema aliyotenda Daudi yalimfanya Suleimani kupona kutoka kwenye hukumu ya Mungu. Kumbe jambo jema laweza kuokoa familia au ukoo; vivyo hivyo laana ya mtu mwovu inaweza kupita kutoka kwa wazazi hadi kwa watoto.

WASIMAMIZI WA LAANA:
Mtu anakuwa na laana; utajiuliza kwanini laana haitoki? Tukisoma katika kitabu Luka 13:10-16 “Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?” Kimsingi kila laana ina pepo anayeisimamia laana hiyo; watu wangemuona miaka 18 kuwa ni mgonjwa kumbe kuna pepo. na ndio maana waweza kumwona mtu kichaa kumbe nyuma yake kuna wasimamizi wa ukichaa.

Pepo waweza kuwa ndani ya mtu au nje ya mtu ili kusimamia laana, na ndio maana waweza kumkutamtu unamwambia twende kanisani ukafunguliwe anakuwa hataki kumbe amesimamiwa na wasimamizi wa laana. Kuna wasimamizi wa kipepo kabisa kwaajili ya kusimamia laana. Na pepo hawa wakiingia ndani ya mtu wanamlazimisha kutenda mambo ya ajabu ili kuitekeleza ile laana.

Wakiwa nje yako wanaweza kukuzuia kwa kuingia ndani ya mtu anayetakiwa kukupa msaada. Vunja laana zote katika JINA LA YESU!!!

Barikiwa!!!!!!!!!!!!!
[akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; WAKOLOSAI 2:14]

UFUFUO NA UZIMA [THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH]
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.

No comments:

Post a Comment